Monday, April 20, 2009

KUTOKA CHUMBA CHA HABARI - RADIO HURUMA


HABARI KWA UFUPI:
NCHI za Tanzania na Rwanda zinatarajia kukuza ushirikiano na kurahisisha muingiliano wa kijamii baina ya wananchi wa nchi hizo mbili baada ya kuundwa kwa chama cha urafiki kati ya Tanzania na Rwanda (TARAFA).

Chama hicho ambacho kitafanya uzinduzi wake hivi karibuni kwa lengo la kukitambulisha Wananchi wa nchi hizo kinatarajia kukuza ushirikiano katika nyanya mbali mbali ikiwemo shughuli za kijamii na kitamaduni.

Ofisa mwenezi wa Chama hicho Godfrey Semwaiko amesema chama hicho ambacho kinaongozwa na Balozi Christopher Liundi ambaye ni Mwenyekiti kina lengo la kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo.

WANANCHI wa Kijiji cha Cheku wilayani Kondoa Mkoani Dodoma wanatarajiwa kuondokana na adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta maji, baada ya kupatikana wafadhili watakagharamia mradi wa maji utakaogharimu zaidi ya shiulingi milioni 60.

Wakazi hao waliokuwa wakisafiri zaidi ya kilomita 10 kuteka maji kwa ajili ya matumizi ya kila siku wataondokana na adha hiyo baada ya wageni kutoka nchini Canada kupitia Shirika la Uhifadhi wa Mazingira na Utamaduni wa Asili wa Kondoa (KICHECO) Mwaka 2006 kutembelea kijijini hapo na kukubali kufadhi mradi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari , Mkurugenzi Mtendaji wa KICHECO, ambaye pia ni Meneja wa Mradi huo, Moshi Changai amesema wageni hao wameamua kufadhili mradi huo baada ya kuona jinsi wakazi wa kijiji hicho wanavyotumia muda mwingi kufuata maji huku wakikwama kufanya shughuli za maendeleo.

NA…..Wafanyakazi wa Mashirika ya Misaada nchini Somalia wanasema kuwa watu wenye silaha wamewateka wenzao watatu, wakiwemo raia mmoja wa Ubelgiji na Mholanzi wanaofanya kazi katika Shirika la Madaktari wasio na mipaka.

Mfanyakazi mwingine wa shirika hilo amesema watu hao watatu walitekwa nyara wakiwa na walinzi wao raia wa Somalia, wakati walipokuwa wakisafiri kuelekea katikati mwa nchi hiyo.

Shirika la Madaktari wasio na Mipaka la Ubelgiji limethibitisha, kupoteza mawaliano na baadhi ya wafanyakazi wake walioko nchini humo.
Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia yamesababisha vifo vya watu kadhaa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, huku wengine zaidi ya milioni tatu wakiishi kwa kutegemea misaada ya chakula.


Source:Chumba cha Habari - Radio Huruma Fm

No comments: