Tuesday, March 31, 2009

Onyo kwa wakuu wa shule na walimu wa vyuo nchini

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, amelalamikia hatua ya baadhi ya watu wanaowarubuni Wakuu wa Shule na Vyuo hapa nchini na kujipatia mamilioni ya shilingi kwa njia ya udanganyifu kwa kutumia jina lake.

Akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu ana Mfunzo ya Ufundi linalofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Nyinda Classic uliopo mtaa wa Bombo Jijini Tanga, jana Profesa Maghembe alisema kuwa watu hao wanafika kwenye hoteli na kuwapigia simu wakuu hao na kujitambulisha kwamba ni Waziri huyo huku wakidai fedha.

Alisema mtu mmoja alifika kwenye hoteli moja mjini Dodoma na kumpigia simu Mkuu wa chuo kimoja wapo mkoani humo na kujitambulisha kwamba ni Waziri huyo na kumtaka mkuu huyo amletee shilingi milioni 5.

Hata hivyo, Waziri huyo hakufafanua wala kueleza kwamba tangu kuzuka kwa suala hilo ni hatua gani amechukua na kwamba watu hao ni kwanini wanatumia jina lake, lakini wachunguzi wa mambo walieleza kwamba tabia hiyo inafanywa pengine kutokana na uchunguzi unaoendelea kwa sasa kwa baadhi ya shule na vyuo vinavyotuhumiwa kuhusika na uzalishaji wa vyeti feki.

Mjumbe mmoja wa baraza hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa hivi sasa kuna timu ya maofisa kutoka wizara ya elimu wakishirikiana na maofisa usalama wa taifa wamekuwa wakipita kwenye shule na vyuo kuwabaini wanafunzi wanaotumia vyeti bandia na vyuo vinavyozalisha vyeti hivyo.

No comments: