Monday, March 30, 2009
Jamani!Jamani this is not good i swear why lakini?
v Mkazi wa Dodoma mjini, Bw. Peter Msangi, amejikuta katika wakati mgumu baada ya familia yake kumtenga kutokana na kuoa mwanamke albino, Bi. Mariam Simon. Ndugu wa Bw. Harusi huyo walisusia sherehe ya kijana wao baada ya kumtaka amwache albino huyo, lakini bila mafanikio. Kutokana na hali hiyo, wazazi walimfukuza kwa madai kuwa amewapelekea nuksi katika familia, kwani tangu ukoo huo umekuwapo duniani haujawahi kuzaa mtoto albino wala kuozesha mtu wa jinsi hiyo. Katika utaratibu mzima wa kuhakikisha anapata jiko, aliwapa taarifa wazazi wake, lakini ilikuwa vigumu kueleweka kwa wazazi wake jambo ambalo lilimfanya ajishughulikie katika suala zima la mahari. Pamoja na kuendelea na hatua hizo zote, wazazi wake waliendelea kumchukia na kumwona kama amechanganyikiwa lakini msimamo wake ulizidi kuwa madhubuti na kutaka kumaliza mahari, ili aweze kupata fursa ya kupangiwa muda wa kuoa. Hata hivyo, juhudi za kuhakikisha anakamilisha hatua zote zilizidi kuwapa hasira wazazi wake ambao waliamua kutotaka kumwona hata kwa sura, kwa madai amewafanyia kitu kibaya. Baada ya wazazi kususia harusi hiyo na kuamua kumfuta katika ukoo, Kanisa liliamua kumtafuta mzazi wa bandia ili kuweza kuondoa maswali mengi kwa watu walioalikwa kufika katika sherehe ambayo ilikuwa ya kufa mtu. Akizungumzia suala hilo Bwana Harusi juu ya uamuzi wake na wa wazazi, alisema amempenda binti huyo ambaye ni albino kwani ana sifa zote za kuitwa mke mwema. Bw. Msangi alisema kuwa anachotambua ni kila mtu ana kasoro zake na kila mtu ni mlemavu, hivyo suala la ngozi haliwezi kuwa kigezo cha kumfanya asimwoe binti huyo ambaye anajua wazi kuwa hakuna binti mzuri kama yeye. “Albino ni mwanadamu kama mwanadamu mwingine na rangi yake imenivutia zaidi kwani hana tofauti na Wazungu," alisema Bw. Msangi ambaye sherehe yake ilikuwa kubwa kuliko kawaida. Juu ya uamuzi wa wazazi kumtenga, alisema anachoshukuru wazazi wake ni kumlea vizuri na kumfundisha mema na mabaya, hivyo kwa kuwa ameishakua amechagua kumwoa mke huyo ambaye ni chaguo la moyo wake. Alisema anachosubiri sasa ni kuona kama wazazi wake watamchukia yeye pekee au watawachukia pia wajukuu kama Mungu atawajalia kupata watoto hapo baadaye. Kwa upande wake, Bibi Harusi, Mariam Saimoni alisema mpango wake na wa Mungu, ni kuona kila mwanamke anaolewa na yeye ameolewa kama walivyo wanawake wengine na kuhusu suala la yeye kuzaliwa albino si lake ni mpango wa Mungu. Alisema kuwa albino si tiketi ya kukosa haki zake, bali anastahili kupata haki zake kama watu wengine na anawashukuru wazazi waliomsomesha na kumfanya aishi maisha mazuri kama watu wengine. Pia alimsifu mumewe kwa ujasiri wa kumchumbia na kufuata taratibu zote kwa uaminifu, mpaka kufikia hatua ya kufunga pingu za maisha ingawa wamekuwa na mapito mengi, kwani alionekana kama anaoa mtu ambaye hastahili kuwa katika jamii.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment