Wednesday, February 24, 2010

KUTOKA CHUMBA CHA HABARI

MOROGORO
v WAANDISHI wa habari tanzania wanakabiliwa na changamoto ya ukutokuwa wabunifu katika kuboresha kazi zao na kuimarisha dhana na maudhui ya sekta ya habari.

Hayo yamesemwa na wakufunzi akiwemo Mhadhili wa chuo kikuu cha Tumaini tawi la Dar es salaam Gad Mkemwa na Meneja Program mstaafu wa shirika la utangazaji nchini TBC,Eda Sanga kwenye mafunzo ya uandishi wa habari za utangazaji mjini Morogoro.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakufunzi hao walisema kuwepo vyombo vingi vya habari si chanzo cha vyombo hivyo kukosa ubunifu badala yake inatakiwa kuwa kigezo cha kuongeza ubunifu ili kuboresha soko la wasikilizaji,watazamaji na wasomaji.

Akizungumzia mada zinazofundishwa ikiwemo ya mbinu mpya za uandishi,matamshi,adabu,tafisiri ya uandishi na jinsi ya kufupisha habari alisema kazi ya uandishi ni ngumu kwakuwa inahitaji kusoma muda wote ili kubadilika.

Eda alisema waandishi wa leo wanatakiwa kuwa wabunifu zaidi katika kazi zao kwakuwa wanavitendea kazi vingi na vyenye kurahisisha kazi zao ukilinganisha na uandishi wa awali.

Awali mweyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoni hapa MOROPC,Bonventure Mtalimbo aliwataka waandishi kubadilika kwa kutokukubali kutumika kama chombo badala yake kuzingatia maadili ya uandishi.

Alisema endapo wataendelea kuwatumikia watu kwa kujali kipato kidogo wanachopewa,wataendelea kufa msikini na fani kuendelea kudharaulika kwa jamii wanayoitumikia ikiitwa fani ya wenye njaa.

Kondoa
v Watu wawili kati ya 94 waliokuwa wamepatwa na ugonjwa wa kipindupindu wamekufa na wengine wametibiwa na kuruhusiwa katika maeneo ya Kikore na Huruwi wilayani Kondoa mkoani Dodoma.

Mganga mkuu wa wilaya ya Kondoa Dkt John Ruanda bila kuwataja majina yao marehemu amesema kuwa kwa sasa amebakia mgonjwa mmoja tu ambaye anaendelea vyema na matibabu hali inayoonyesha kuwa kipindupindu kitakuwa kimedhibitiwa ipasavyo.

Dkt Ruanda amesema kuwa hali ya milipuko ya magonjwa yatokanayo na uchafu ukiwemo ugonjwa wa kipindupindu ni matokeo ya watu wengi kudharau maagizo ya wataalamu wanapotoa elimu ya kupambana na magonjwa hayo.

Amesema kwa uchunguzi uliofanywa katika maeneo ya Bolisa ulipoanzia ugonjwa wa kipindupindu mwishoni mwa mwaka jana eneo ambalo pia ni maarufu sana kwa matunda ya aina mbalimbali,watu hawatumii vyoo ipasavyo.

Amebainisha kuwa hata kama familia inacho choo bado kuna wanafamilia hiyo wanadiriki kujisaidia katika maeneo karibu na miti ya matunda wanayovuna na kuyala bila kunawa na kuyaosha na hayohayo huyapeleka sokoni.

Amesisitiza kuwa katika maeneo ya Kikore kulikotokea vifo,kunalo tatizo la maji safi na salama lakini katika kipindi hiki cha mvua watu wanakunywa maji machafu na mengine ya madimbwini yasiyochemshwa.

Amewataka wananchi wilayani Kondoa kupitia kwa viongozi wao kama madiwani wahakikishe kuwa suala la afya si la mzaha bali ni suala nyeti linalohitaji umakini wa hali ya juu ili kunusuru afya.

Alisema dharau na kujipa moyo na matumaini yasiyoendana na hali halisi ya matokeo ya madhara ya kuzuka kwa ugonjwa,husababisha kilio kwani kama ni mtu kupoteza maisha huwa hakujaribiwi wala hakurudiwi akishakufa kafa tu.

WAKATI HUO HUO: Wananchi wa maeneo ambayo yamefyekwa mazao yaliyokuwa yamekatazwa kulimwa kwa kile kilichodaiwa na mamlaka ya mji mdogo wa Kondoa kuwa ni hifadhi ya wezi,vibaka na majambazi,wametishia kutopiga kura mwaka huu kutokana na kudharauliwa na kuelekezwa kwenye maangamizi ya njaa.

Wakizungumza kwa hasira kwa nyakati tofauti kwenye maeneo ya Kwapakacha,Kilimani,Fockland na Magodawn wananchi hao wameelezea kushangazwa kwao na hatua hiyo ya mamlaka ya mji mdogo wa Kondoa kuwafyekea mazao yao yaliyokomaa huku wakiwa hawana wanachotegemea.

Mmoja wa wazee wa siku nyingi ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka takriban 80 Khamisi Mwasi yeye kwa upande wake alinukuu kauli za hayati baba wa Taifa mwalimu Nyerere kuwa kauli ya kilimo cha kufa na kupona watu walihimizwa kulima hata pembezoni mwa nyumba zao au ofisi mwaka 1972 hata wabakize vinjia tu vya kupita ili kukabiliana na balaa njaa lakini leo serikali inakubali wananchi wanaharibiwa mazao yeo.

Mzee Mwasi alihoji kama mazao yanayorefuka yanaweza kuwa vichaka vya wahalifu,je vichaka vya asili ambavyo hadi sasa ni vingi tena kwenye barabara za mamlaka hiyohiyo ya mji mdogo wa Kondoa mbona havitolewi wakati vyenyewe ndimo huwa kunakutwa hata mali za wizi.


Walisema mazao ya chakula tena kwa ajili ya kujikimu tu yangeachwa yakomae kwa kuwa ni ya muda yatolewe na wao serikali wahakkikishe wanaondoa vichaka vya asili amabvyo ndiyo maficho hasa ya vibaka na wezi au hata ubakaji nyakati za usiku.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kilimani Shaabani Boi yeye kwa upande wake alipohojiwa na mwanahabari hizi watawatulizaje wananchi hao alijigamba kuwa viongozi wametekeleza agizo lao na kwamba wanaopingana na agizo hilo ni wachache hivyo suala la kutopiga kura ni tishio dogo sana kwani wanaokubaliana na uamuzi huo ni wengi.

Mkurugenzi wa mamlaka ya mji mdogo wa Kondoa Anold Jidai yeye kwa upande wake alisisitiza kuwa agizo hilo ni maamuzi ya wajumbe wa baraza la mamlaka ya mji mdogo wa Kondoa wala si maamuzi ya mtu mmoja hivyo utekelezaji ni lazima.

Kwa upande wake serikali ya wilaya ya Kondoa inafanya jitihada za kupata chakula kutoka serikali kuu ili kuwanusuru wananchi katika baadhi ya maeneo ya wilaya hii ya Kondoa ambao wanakabiliwa na hali ya njaa.

Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya ya Kondoa Saidi Bwanamdogo,hata baada ya ugawaji wa chakula cha njaa awamu ya kwanza,bado uchunguzi unaonyesha kuwa kunayo baadhi ya maeneo ambayo yanakabiliwa na tatizo la njaa.

No comments: